The Best of Hyogo ~ひょうごの魅力「再」発見ツアー~
 

FURSA YA KUONA SHUGHULI, MAZINGIRA NA VIVUTIO VYA JAPANI VIJIJINI: SAFARI KWENDA MJI WA TAKA (Takacho).

SHUBI MATOVELO's visit to HARIMA
Name SHUBI MATOVELO
From TANZANIA
Time in Japan 11 MONTHS
visited day 2017/02/23 - 2017/02/24
area TAKACHO
HARIMA
"FURSA YA KUONA SHUGHULI, MAZINGIRA NA VIVUTIO VYA JAPANI VIJIJINI: SAFARI KWENDA MJI WA TAKA (Takacho)."
2017/02/23 - 2017/02/24
シュビ2

Kupitia mwalimu wangu wa lugha ya Kijapani nilipata tangazo la fursa ya safari ya siku mbili kwenda kutembelea mji mdogo wa Taka na kubahatika kushiriki safari hii. Mji huu upo ndani ya prifekcha/mkoa wa Hyogo na kaskazini mwa jiji la Kobe, takribani mwendo wa saa moja na robo kwa basi. Baada ya kuishi jijini Kobe kwa miezi 11 sasa na kuona na kuzoea maisha katika mji wa kisasa fursa ya kuzuru na kuona maisha katika mji mdogo, kulinganisha maisha ya maeneo ya mashambani na mjini ilikuja wakati muafaka.

Kama ilivyo kwa maeneo kadhaa ya Japani vijijini, idadi ya wakazi katika mji wa Taka imekuwa ikipungua katika miaka ya hivi karibuni. Idadi ya watu wanaozaliwa au kuhamia ikiwa ni ndogo kuliko ya wanaoondoka hali ambayo inaathiri ukuaji wa mji huu na ambayo inatishia uhai wa mji kama ikiachwa kuendelea. Mji huu wa Taka pia, haufahamiki sana hata na wajapani waliozaliwa au wanaoishi ndani ya mkoa huu wa Hyogo. Safari hii ilikuwa moja ya jitihada za mamlaka ya mji wa Taka na mkoa wa Hyogo kwa ujumla kuutangaza mji huu na vivutio vyake hata hatimaye watu wengi zaidi na zaidi, wageni kwa wenyeji wafikirie kuutembelea mji huu au kuhamishia makazi yao huko mambo ambayo yanaweza kuhuisha ukuaji wa mji wa Taka.

Waandaaji wa safari hii walitupa kazi, kama wageni, ya kuangalia mazingira, vivutio, baadhi ya shughuli zinazofanywa na wenyeji, kuongea na wenyeji na baada ya hapo kuwapa maoni yetu kuhusu namna wanavyoweza kufanya kuvutia wageni na kupendekeza maandalizi yatakayohitajika, na mpangilio wa ziara mathalan kwa wageni wanaokuja kwa matembezi ya siku moja ama mbili.


Katika Makala hii naandika kwa ufupi vivutio nilivyoona na baadhi ya mambo niliyojifunza na kufanya katika ziara hii.


1. Kutengeneza Tofu
Tofu ni chakula maarufu sana Japani, kinatengenezwa kutokana na maharage ya soya. Tulielezwa hatua zote za utengenezaji wa chakula hiki, kisha katika jengo maalum kwa kuoneshea
utengenezaji wa chakula hiki niliona na kushiriki katika utengenezaji wa tofu na baada ya hapo kuonja tofu ambayo ndio kwanza imetoka kutengenezwa. Ilikuwa kitu cha kuvutia kuona mubashara utengenezaji wa chakula hiki ambacho nimekuwa nakiona kikitumika katika milo karibu yote tangia nimefika Japani

シュビ3

シュビ4


2. Kutengeneza na kuonja “Makizushi”
Makizushi pia ni kitu cha kula. Ni mkusanyiko wa wali, kipande cha tango kilichokatwa kwa urefu, vipande vya uyoga na aina maalum ya mboga inayopatikana Taka. Vitu hivi vinatandazwa juu ya karatasi maalum inayolika, inayotokana na majani yaliyokaushwa na kufanywa kama karatasi, kisha kwa pamoja vinaviringishwa ndani ya karatasi hii kufanya “roll” ambayo inakatwa katika vipande vidogo tayari kuliwa. Hii ilikuwa mara yangu ya kwanza kula makizushi, ilikuwa tamu sana. Tulielezwa, duka hili la makizushi pale Taka ni maarufu sana kwa wakazi wa hapo na maeneo ya karibu. Walitukaribisha na kutufundisha namna ya kutengeneza makizushi na kila mmoja akajitengenezea makizushi yake kwa chakula cha mchana.

シュビ5

シュビ6


3. Kutengeneza karatasi ya asili ya Japani (Washi)
Washi ni karatasi ya kijapani ya asili. Mji wa Taka unazalisha sehemu kubwa sana ya karatasi hizi kwa matumizi Japani kote. Japo karatasi hizi hazitumiki kwa matumizi ya kila siku lakini bado zinatumika kwa matumizi maalum kama kutengenezea vyeti vya kielimu au bahasha za matumizi maalum na kadhalika. Tulijifunza hatua zote tangu uvunaji wa miti inayotumika kama malighafi mpaka inapokuwa karatasi na kila mmoja alishiriki kwa vitendo hatua za mwishoni za utengenezaji na kujitengenezea karatasi yake mwenyewe ambazo mwishowe tulipewa kama zawadi. Ilikuwa kitu cha kuvutia sana kuona karatasi inatokeza kutoka uji uji wa ngozi ya mti ulipondwa. Cha kuvutia zaidi ni utumiaji wa vifaa rahisi na namna zile zile za kiasili bila kuhitaji kemikali au vifaa ghali.

シュビ7


4. Bustani za Lavenda
Mji huu pia una bustani za mmea wa lavenda na kituo ambapo wanatengeneza bidhaa mbali mbali kama manukato, mafuta ya viganja, sabuni, mishumaa na mapambo zinazotumia mmea huu. Tulipata fursa ya kujifunza kwa vitendo utengenezaji wa manukato na mafuta ya kiganja na kila mmoja akajipatia chupa ya manukato na mafuta hayo. Katika nchi iliyoendelea ambapo bidhaa nyingi zinaengenezwa kwa mitambo viwandani kupata fursa ya kutumia njia rahisi za mikono kutengeneza bidhaa kama hizi ni kitu kinavutia.

シュビ8


5. Matembezi-uzima (Wellness walking)
Pamoja na kwamba, kwa Japani, hata mijini ni rahisi na salama kufanya matembezi kwa sababu ya miundo mbinu inayozingatia waenda kwa miguu, kuna utulivu na hali ya starehe kutembea ukiwa umezungukwa na mazingia asili ya kimsitu msitu. Katika mji wa Taka wametenga mahala ambapo watu wanaweza kwenda kwa matembezi kwenye njia iliyo ndani ya msitu katika mwinuko wa mlima. Nilivutiwa na vitu viwili vikubwa, cha kwanza ni kuunganisha matembezi na fursa ya kupima shinikizo la damu na mapigo ya moyo kabla ya matembezi na kuendelea kuangaliza kubadilika kwa mapigo ya moyo kadri tulivyoendelea kutembea. Pili, ilikuwa ni ule wasaa wa kutandika mkeka maalum wa yoga juu ya magogo yaliyolazwa katikati ya msitu kama mfano wa kitanda na kujilaza ndani ya msitu, katikati ya miti. kupumzika huku unatazama miti mirefu ikiyumba kwa madaha kufuata upepo ilikuwa starehe ya namna yake.

シュビ9

シュビ10


Mji huu wa Taka ambao umezungukwa na safu za milima ukiwa na vitongoji vilivyojengwa viki ambaa ambaa pembezoni mwa mto, katikati ya mabonde (penye miguu) ya milima hii huku nyumba za wakazi wengi zikiwa zimezungukwa na mashamba ya mpunga ni mahala pazuri kutembelea na kuona mazingira, maisha, shughuli na vivutio vya miji ya mashambani, vionjo tofauti na vile maarufu vya mijini kama Kobe ama Osaka.

シュビ11


Kihusishi.
Kwa taarifa zaidi, bofya kihusishi hapo chini

Ukurasa wa tovuti wa Takacho
多可町HP


 
 
「本サイトに掲載されている画像・文章等の無断転載、引用を禁じます。」 Copyright(C) Hyogo International Association AllRights Reserved.